SEMINA YA UCHUMBA NA NDOA-T.E.C KURASINI-25 Januari 2014
UTOTO, UJANA, MAHUSIANO YA UCHUMBA NA NDOA
Imetayarishwa na
Prof. Emil N. Kikwilu
kwa ajili ya semina ya “Ujana, Mahusiano ya Uchumba na Ndoa” iliyofanyika katika ukumbi wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Kurasini,
tarehe 25 Januari 2014
1. UTOTO NA UJANA
2. Utoto ni umri wa kutegemea wazazi au watu wengine, umri wa kuiga kila kitu mtoto anachoona wengine wanakifanya, umri wa kufurahia mtoto akifanya kile alichofanya mwingine. Ni umri uliyojaa furaha na hudhini za muda mfupi. Ni umri usiojali muda ujao, sasa ni sasa, na sasa ndio wakati muafaka.
3. Ujana ni umri wenye nguvu (energetic), tamaa nyingi (wishful thinking), na malengo makubwa (big/high targets). Ni umri unaotaka matokeo makubwa sasa (Big results now!!). Ni umri usio na subira (Inpatient age). Ni umri wa kutojiamini sana (dependence) au kujiamini sana (independence).
4. Matokeo ya malezi ya familia wakati wa utoto na misukumo ya ujana husababisha kupata watu wenye milengo mikuu minne (attitude dispositions) kama ilivyoainishwa katika jedwali hapo chini.
I’M OK – YOU’RE OK: (The winner) ü High self-esteem ü Respects others ü Self-confident ü Accepts positive feedback ü Gives positive feedback ü Expects others to succeed ü Not-judgemental ü Non-offensive ü Seeks win-win solutions | I’M OK – YOU’RE NOT OK: (The arrogant) · High self-esteem · Overbearing · Bossy · Highly evaluative of others · Impatient · Hostile · Task-oriented |
I’M NOT OK – YOU’RE OK: (The Sucker) Ø Low self-esteem Ø Difficulty accepting positive feedback Ø Unassertive Ø Worrisome Ø Assumes own fault | I’M NOT OK – YOU’RE NOT OK: (The Loser) Low self-esteem Feelings of helplessness and hopelessness Blames others and world Nothing matters Expects to fail |
5. Kila mtu ingependeza kama akiwa na mlengo wa “I’M OK, YOU’RE OK!” Kila mtu anaweza kujifunza na akawa na mlengo wa “I’M OK, YOU’RE OK!” Heri yao walio na mlengo wa “I’M OK, YOU’RE OK! Tufanyeje ili tuwe na mlengo wa kuleta tija katika maisha na hata familia? (yaani mlengo wa “I’M OK, YOU’RE OK!”)
6. Utoto na Ujana unahitaji malezi (moderation/guidance). Tatizo: Kila mtu huona kuwa njia yake inafaa au matendo yake ndio sahihi (Mithali 16: 2a). Kama baba/mama yako ni wa mlengo fulani, atakulea katika mlengo huo huo. Hii ni kwa sababu mtu hutengeneza mahusiano na wenzake, na kila mtu hutengeneza anachokiweza!
7. Ni nani atatuhakikishia kuwa tunakuwa na mlengo wa kuleta tija kwa familia? Hapa ndipo tunahitaji mshauri ajuae yote! Mungu mwenyewe ndiye anayeweza kutufundisha/kutulea! Hata kama umezeeka kama mimi unaweza kubadilika na kuwa na mlengo wa kuleta tija kwa familia. Hakuna kisichowezekana kwa Mungu (Luka 1:37), na pia Mungu hufanya kazi pamoja na wateule wake katika kuwapatia mema (Warumi 8:28), kwa sababu Mungu hujishughulisha sana na mambo yetu (1Petro 5:7).
8. UCHUMBA
9. Uchumba ni mkataba/makubaliano kati ya mwanaume (mvulana) na mwanamke (msichana) yanayolenga matayarisho ya kufunga ndoa. Ni makubaliano yanayotoa matarajio kwamba iko siku hawa wawili watakuja kuwa wamoja au kuishi pamoja kama mume na mke. Neno la Mungu linatuambia “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja (Mwanzo 2:24). Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja (Mathayo 19:6a).” Uchumba hujenga matarajio ya kufunga ndoa/ kuishi pamoja kama mume na mke/kuwa mwili mmoja. Kimsingi ni matayarisho ya mvulana na msichana ya kuwa waanzilishi wa familia mpya kwa lengo la kuzaa na kulea watoto (propagation of species) (Mwanzo 1:28). Matarajio huleta hamu ya kupata kabisa. Kila mchumba hujitahidi kumpendeza mwenzake ili hatimaye wafunge ndoa/waishi pamoja/wawe mwili mmoja.
10. Tatizo la kwanza: Je, mchumba anampendeza mwenzake kwa namna gani? Kwa kuonyesha tabia yake au kwa kuificha? Kama kweli wachumba wangetambua kwamba wanajiandaa kuwa mwili mmoja, wangejitahidi kuonyesha tabia zao kama zilivyo kwa sababu kutegemea kuchanganya maji na mafuta ni uendawazimu! Hata ukikoroga kwa nguvu namna gani, utakapoacha kukoroga yatatengana tu! (Rejea jedwali letu hapo juu).
11. Tatizo la pili: Kwa nini unataka huyu awe mchumba wako na sio yule? Je umwonavyo, ndivyo alivyo? Je umwonavyo ndivyo atakuwa miaka yote ya ndoa? Kama ukisema unampenda, je unampenda yeye, au unapenda mwili wake! Au miondoko yake, au sauti yake! Au kwa sababu uliambiwa na wenzako kwamba mzuri ni aliye na umbo hili! Au kwa sababu ana umbo dogo, hivyo ni rahisi kumuonea! Au ni kwa sababu siku ya harusi utaambiwa umnyenyue mwenzio na mpige picha (kama ni mzito sana utaaibika kwa sababu utaanguka naye kabla picha hazijapigwa!). Au, huyu hata nikitembea naye mtaani watu watanipongeza kwa kuchagua mke/mume mzuri! Kumbuka msemo huu “Beauty = (distance*dress*foolishness of the observer!)”. Tatizo hili linakuja kuleta madhara baada ya kufunga ndoa kwa sababu mabadiliko humpata kila mtu! Mwembamba anaweza kunenepa, mnene anaweza kukonda, uzuri utafifia, nguvu zitaisha, sauti itabadilika. Kuna kupata ajali na kupoteza kiungo au viungo. Kuna mabadiliko baada ya kuzaa mtoto/watoto, nk.
12. Kwa kuwa uchumba ni mkataba/makubaliano ya kujifahamu kwa undani, basi uchumba unaweza kuvunjwa, kama mmoja wao anaona hataweza kuishi kama mwanandoa na mwenzi wake. Hii ina maana kwamba si kila uchumba huendelea hadi kufikia ndoa! Tukisema kwamba kila uchumba huendelea hadi ndoa, tutakuwa tunaua faida ya uchumba.
13. Mahusiano ya uchumba:
14. Mahusiano ya uchumba yanayoleta ndoa ya kudumu ni rahisi sana. Yanahitaji kujionyesha kwa mchumba wako kama ulivyo bila kujificha na yeye ajionyeshe kwako kama alivyo bila kuficha. (Huku ndiyo kumpendeza mchumba wako! Hayo ndiyo mahusiano sahihi ya uchumba!). Ni mahusiano ya kuhakikisha kwamba mchumba wako anakujua kama ulivyo na wewe umjue kama alivyo. Uhusiano wa uchumba si wa kuigiza. Kipindi cha uchumba ni cha kujua mwenzako anapenda nini, na anachukia nini. Ni kipindi cha kuamua kama upo tayari kuishi na mwezio kama alivyo. Ni kipindi cha kuelezana vitu ambavyo unapenda au hupendi. Ni kipindi cha kuelezana malengo yenu, na spidi ya kuyafikia malengo hayo. (Ukisikia mume au mke anahadithia wenzake kwamba “Mume wangu/mke wangu, utadhani hajasoma!” Hii ni dalili kwamba wakati wa uchumba watu hawa hawakujifunua vizuri!) Kuna utani uliokuwa unatolewa wakati tukiwa chuo kwa wasichana wa Kichaga: “Yesu na Maria!, Yaani we Baba Kimaro umeshindwa hata kuiba kazini tupate hela tufanyie mambo yetu? Hawa hawakujiweka wazi katika spidi ya kupata maendeleo. Au mke alikuwa na matarajio makubwa na huyu mume isivyo. Hakumjua vizuri. Mchumba anakuwa na wema wa kupitiliza, kumbe moyoni anajikaza tu, anaigiza kuwa mwema! Iko siku baada ya kufunga ndoa yatakushinda tu, na mwenzi wako atakata tamaa au atasema penzi lako limeelekezwa kwa mpenzi mwingine. Kumbe sivyo, bali uliigiza wema usiokuwa wako wakati wa uchumba!
15. Tatizo kubwa kama tulivyoona katika kifungu cha 10 hapo juu, ni kwamba wachumba hujitahidi kuficha tabia zao, mitazamo yao, matamanio yao, malengo yao, nk. Kwa lugha nyepesi wachumba wengi huigiza maisha ya kuwapendeza wenzi wao.
16. Swali: Utajuaje kwamba mchumba wako anajionyesha kwako kama alivyo? Utafanyaje ili mchumba wako ajifunue kwako kama alivyo?
17. Hapa ndipo tunahitaji mshauri ajuae yote! Mungu mwenyewe ndiye anayejua mchumba wako atakayeishi nawe kwa ufanisi wakati wa ndoa, hapa duniani na mbinguni! Ndiye anayetaka kukuonyesha mchumba wa namna hiyo, na ni wapi alipo, na namna ya kumpata!
18. Kwa bahati mbaya, Shetani naye anajua mchumba wako atakayeishi nawe kwa ufanisi wakati wa ndoa! Lakini hapendi hata kidogo umjue ni nani na alipo! Kwa hiyo shetani atajitahidi kukuelekeza kwa mchumba feki ili uharibikiwe katika maisha ya sasa na maisha ya milele! (Yesu anadhihirisha hili katika Injili ya Yohane sura ya 10, aya ya 10, anasema “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele”) (Yohane 10:10).
19. Wakati natafuta mchumba nilikuwa ninasali na kuomba Mungu anipatie mchumba tutakaeishi kwa amani. Nilifanya hivyo kwa muda mrefu na kwa bidii mno kiasi kwamba siku moja nilitembea toka Muhimbili kuelekea Kariakoo, nikavuka barabara ya Morogoro Road bila kujitambua. Yaani sikujua kwamba navuka barabara yenye magari mengi kama hiyo. Na nilipojitambua, nilikuwa nimevuka tayari. Nikamshukuru Mungu kwa kuniepusha na ajali. Hakika malaika wake alinilinda na anaendelea kunilinda hadi leo, ingawa mimi ni Mdhaifu sana katika kushukuru!
20. Mifano hai: Tulivyojenga uchumba. Mfano wa uchumba ulioshindikana. Mfano wa uchumba uliofanikiwa.
21. Madhara ya kuficha tabia, unachopenda, malengo na matamanio (madhara ya kuigiza wakati wa uchumba): Si rahisi kuishi kwa kuigiza maisha yako yote, la sivyo maisha yatakuwa magumu kwako. Mara nyingi baada ya kufunga ndoa, watu huacha kuficha tabia zao, huanza kuonyesha malengo na matazamio yao. Kama kimoja au vyote vikionekana tofauti na vya mwenzio, misuguano huanza kwa kasi. Hapa ndipo panahitajika milengo ya I’M OK, YOU’ARE OK, la sivyo ugonvi huanza, na inakuwa wote mmechelewa kubadilisha maamuzi (Ndoa ya Kikatoliki haichezewi ovyo, ni Sakramenti!)
22. Heri yao walio na mlengo wa “I’M OK, YOU’RE OK na wakapata wachumba ambao wana mlengo huo huo kwa sababu hawa wanaweza kurekebishana au kukubaliana! Miunganiko mingine ya milengo ni matatizo matupu! Hubomoa uchumba na ndoa pia. Huchelewesha maendeleo ya familia, na inaweza kuzuia kabisa maendeleo ya familia. Kuna wanandoa wengi wanaoishi kwa hudhuni maisha yao yote kwa sababu wamefunga ndoa na mwenzi wao ambaye hawapatani milengo. Kuna wanandoa wengine wamehalalisha hata vitu vinavyoitwa nyumba ndogo kwa sababu hiyo hiyo.
23. NDOA
24. Ndoa ni muungano wa watu wawili (mwanamume na mwanamke) waliokubaliana kuishi kama mume na mke. Katika kanisa, lazima wawe wamejitambulisha kwa kanisa kwamba wataishi kama mume na mke kwa tendo la Sakramenti ya ndoa. Tendo hilo huitwa kufunga ndoa. Sakramenti ya ndoa katika Kanisa Katoliki haibatilishwi kirahisi kwa sababu Yesu mwenyewe alitamka “Basi, aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe” (Mathayo 19:6b).
25. Ili mambo yaende sawa, kijana (mvulana au msichana) hana bidi kuanza na uchumba kwa maana ya kujifunza tabia ya mwenzi wake. Hii itamwezesha kufanya maamuzi magumu, yasiyobatilishwa na binadamu, ila Mungu tu. Yaani Kufunga ndoa. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo, lazima kumuomba Mungu anayejua mchumba wako alipo! Hakuna mkato. Nimeona ndoa zilizofungwa Jumamosi na kusherehekewa usiku kucha, na Jumapili wana ndoa hao wapya wakatalikiana! Aibu kubwa kwa wazazi na kwa Kanisa husika!
26. Mahusiano ya ndoa (Mahusiano baada ya kufunga ndoa)
27. Mahusiano ya ndoa ni lazima yawe ya kupendana. Mapendo ya kweli (Real Love! True Love!). Sio mapendo yanayoamshwa na tamaa ya kujamiiana (Sexually driven love!). Lazima yawe maisha ya kutii Amri Kuu ya Pili ya Mungu kama ilivyo ainishwa katika Injili ya Mathayo sura ya 22 aya ya 39. “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” (Mathayo 22:39). Siku iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alifanya mkutano mkuu na wanafunzi wake. Katika mkutano huo, aliwaagiza kupendana kama alivyowapenda wao na sisi (Yohane 15:12-13). Yesu alitupenda upeo hata akatoa maisha yake msalabani kwa ajili yetu sisi. Upendo kama huo, ndio aliagiza wafuasi wake kupendana vivyo hivyo. Na wewe unayejiita kwa jina lake yaani Mkristo, unaagizwa kumpenda mwenzi wako kama Yesu alivyokupenda wewe!
28. Ni vitu gani vinavyoonyesha kwamba mwanandoa ana upendo wa kweli kwa mwenzi wake? Tufanyeje ili wanandoa tuwe na upendo wa kweli kwa wenzi wetu? Kuna mambo mawili makuu.
29. Kwanza lazima kuwa watu wenye subira (patient). Mtume Paulo anasisitiza maisha ya namna hiyo katika Waraka wake kwa Waefeso sura ya 4 aya ya 1-2. Anasema: “Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo.” Na katika barua yake ya kwanza kwa Wakorintho, alipokuwa anawaonya kwa sababu walikuwa wametilia mkazo mno karama ya kunena kwa lugha, na kudharau karama nyingine, Paulo anasema kuna karama kuu tatu: Imani, Tumaini, Upendo, na katika hayo lililo kuu ni upedo. (Wakorintho 13:13). Anafafanua sifa za upendo: “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabali, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote, hustahimili yote.” (1Wakorintho 13:4-7). Kwa hiyo, katika ndoa, lazima subira itawale!
30. Ukiwa na subira (patient) hukasiriki haraka unapopata “kichocheo kibaya” (negative situation). Hurukii mambo haraka, hupandishi sauti, hugombi. Badala yake unakuwa mpole, unazungumza kwa upole, unaonyesha upendo kwa mwenzi wako na unavumilia maumivu uliyoyapata kutokana na kichocheo kibaya. “When you choose to be patient you respond in a positive way to a negative situation. You are slow to anger. You choose to have a long fuse instead of a quick temper. Instead of demanding, say an explanation, you choose to settle down and extend mercy to your spouse.” Kumbuka kuwa hakuna binadamu yeyote anayependa kuwa karibu na mtu asiye na subira. Ukikosa subura utakuwa na hasira zisizo na kiasi (overreact), za kipumbavu na za kuleta majuto baadaye. Hasira mara zote hazifanyi mambo kuwa mazuri au nafuu, badala yake huzalisha matatizo mengine. Ndoa yenye mwanandoa asiye na subira, ni ndoa isiyo na hadhi wala amani kwa sababu ugonvi utatokea mara kwa mara, na majirani hawakawii kuipa jina baya ndoa/familia ya namna hii! (Mavuvuzela au vuvuzela kaja, hatulali leo, au hatuna pesa za kwenda kuangalia sinema, tunashukuru mara kwa mara tunaonyeshwa sinema ya bure!).
31. Uvumilivu unaotokana na subira unakufanya umpe mwenzi wako nafasi ya kuonekana binadamu. Uvumilivu unaelewa kwamba kila binadamu (pamoja na wewe) hufanya makosa au hushindwa hapa na pale.
32. Uvumilivu unakufanya uwe na busara. Suleimani alisema “Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi, bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu” (Mithali 14:29). Na Paulo alipowaandikia barua Wakolosai alisema: “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake, kama Bwana alivyowasamehe nyinyi, vivyo na ninyi.” (Wakolosai 3:12-13). Naye Petro katika waraka wake wa kwanza anawasihi waume kuishi na wake zao vizuri, anasema “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe.” (1Petro 3:7). Kwa maonyo ya Petro, mume anayemchukiza mke, anayemwonea mke, asiyemstahi mke hawezi kuomba kwa Mungu na akasikiwa. Maombi yake ni chukizo mbele za Mungu Muumba wake! (His prayer is abomination to God!). Si mume tu! Hata mke anayemdharau mume wake, hampi heshima inayostahili, mchokozi anayeleta aibu katika familia, naye maombi yake ni chukizo kwa Mungu wake! (Her prayer is abomination to God!) Asitegemee kupata kitu alichoomba kwa Mungu.
33. Pili lazima tuwe watu wema (kind). Paulo pia nashauri na kutia mkazo umuhimu wa kuwa wema katika barua yake kwa Waefeso sura ya 4 aya ya 32. Anasema: “Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” (Waefeso 4:32) Na mtunga Mithali anasema “Rehema na kweli zisifarakane na wewe; zifunge shingoni mwako, ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri mbele ya Mungu na mbele ya mwanadamu.” (Mithali 3:3-4). Wataalamu wa mapenzi wanasema “Wema ni upendo katika vitendo.” (Kindness is love in action.). Wema unakufanya upendwe au upendeke. Unapokuwa mwema, watu hupenda kuwa karibu nawe.
34. Wema una sifa kuu nne: kuwa na upole (gentleness); kuwa wa msaada/fadhili (helpfuness); utayari wa kutaka/kukubali (willingness); na kuwa tayari kujituma (initiative).
35. Mwanandoa mpole (gentle) si mkali kwa mwezi wake, anachangua lugha na matendo yasiyoweza kumuumiza mwenzi wake.
36. Mwanandoa wa msaada/mfadhili (helping) anajitahidi kutimiza mahitaji ya wakati uliyopo. Kama ni kazi za nyumbani zifanye kwa bidii, kama ni kumsikiliza mwenzi wako msikilize kweli kweli. Kuwa wa msaada kwa mwenzi wako ni kujitahidi kujua hitaji la mwenzi wako na kuwa wa kwanza kulitimiza. Hata kama hitaji lako litaachwa au kusubiri. Mfano: Mmekaa, halafu mke wako anasema “Nina kiu!” Mume mwenye kusaidia ataondoka mara na kuleta glass ya maji baridi, na kumpa mke wake!
37. Mwanandoa mwenye utayari wa kutaka au kukubali (willing) hakatai ombi au wazo la mwenzi wake. Haonyeshi ubabe, havuti miguu kutekeleza kitu, anashirikiana na sio mgumu wa kubadilika inapobidi. Anakubali kukosa na kupata (Win-win situation).
38. Mwanandoa ambaye yuko tayari kujituma huwaza ya mbele, na kuwa wa kwanza kutenda. Hakai kusubiri kusukumwa au kukumbushwa, huwa wa kwanza kumsalimu mwenzi wake, kutabasamu kwanza, kuhudumia kwanza, husamehe kwanza. Kuwa wa kwanza kuonyesha upendo. Ukiona hitaji kwa mwenzi wako, timiza hitaji hilo kwanza, bila kuchelewa.
39. Kama misingi hii ya subira na wema ikijengwe vizuri, basi mambo mengine yanayoharibu mahusiano katika ndoa yatatoweka. Mambo hayo ni: uchoyo (selfishness), ufidhuli (rudeness), uchokozi (irritation), kutoaminiana (disbelieve), wivu (jealousness), masharti (conditions), ushindani (not letting others win), nk,
40. Sio tu kwamba mambo yanayoharibu mahusiano yatatoweka, bali mambo yanayo lea mahusiano yatashamiri. Mambo yanayolea uhusiano wa ndoa ni kama yafuatayo: kumuwazia mwenzi wako (thinking about your spouse); kuonyesha upendo na furaha (good impressions); kumfurahia mwenzi wako (delight in your spouse) (Mhubiri anasema “Uishi kwa furaha na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu ya maisha, na katika taabu zako ulizotaabika chini ya jua.” (Mhubiri 9:9); heshima (honor) (Mambo ya zinaa, nyumba ndogo yasisikiwe katika ndoa yako); kusali (prayers) na kuombeana (pray for your mate); kuwa karibu (intimacy) na kuheshimiana kwa ukaribu huo. Mwiko kusema mambo ya ndani ya nyumba (never gossip about your wife/husband to a friend); kumwelewa mwenzi wako (understand your mate).
41. La mwisho na muhumu sana, ni kuwa Mkristo wa kweli. Ndoa ni Sakramenti. Kuiishi sakramenti hii inahitaji nguvu za kimungu. There is no joy in half hearted Christian life! Wakristo wengi tunataka kuonekana watakatifu mbele za watu hasa wakristo wenzetu, lakini gizani tupo tofauti na utakatifu! Tumekwamia jangwani Sinai, tunakumbuka tuliyoyafanya na kufaidi Misri, hatujafika kwenye nchi ya ahadi –Kaanani, na tunasahau kwamba furaha ya Bwana wetu ndio nguvu zetu! (Soma Waisraeli walivyokuwa wakinung’unika kule jangwani (Hesabu 11:5-6) badala ya kufurahi kwamba wanaelekea kwenye nchi walioahidiwa na Mungu kwamba angewapa -Nchi pana iliyojaa asali na maziwa – Kaanani (Kutoka 3:8). Kumbe wakristo tunatakiwa tuone kwamba furaha ya Bwana wetu Yesu Kristo ndiyo nguvu yetu, kama Nehemia alivyowatuliza Waisraeli walipoanza kulia baada ya kusomewa torati (Nehemia 8:10). Wakristo tunahitaji kujisalimisha kwa Yesu Kristo aliye Bwana na Mwokozi wetu ili aongoze maisha yetu. Mwinjili Yohane anasema Yesu alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio Jina lake. Waliozaliwa si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu. (Yohane 1:11-13).
42. Kuna mambo mengi yanayohusu maisha ya ndoa na uhusiano ufaao. Tukipata muda mwingine titazungumza tena.
43. NAOMBANIISHIE HAPA. MUNGU AWABARIKI SANA, NA AWAPE ROHO YA HEKIMA NA YA UFUNUO KATIKA KUMJUA YEYE. MACHO YA MIOYO YENU YATIWE NURU MJUE TUMAINI LA MWITO WAKE JINSI LILIVYO; NA UTAJIRI WA UTUKUFU WA URITHI WAKE KATIKA WATAKATIFU JINSI ULIVYO; NA UBORA WA UKUU WA UWEZA WAKE NDANI YETU TUAMINIO JINSI ULIVYO….(Waefeso 1:17-19).
44. Tumshukuru Mungu aliyetustahilisha yote haya!!
0 comments:
Post a Comment